Wanaosema biashara ni mchezo wa kubahatisha ni wale wasiojua kuwa biashara ni gurudumu linaloendeshwa kwa kutumia sayansi na sanaa ndani yake. Taarifa ile ile uliyonayo wewe inaweza kumpa matokeo tofauti mwingine, hii yote inategemea kiwango cha ubunifu na unyumbulifu wa kila mmoja.
Kila mmoja anatamani biashara yake iwe ya kwanza kwenye akili ya mteja, lakini hilo haliwezekani kama hatutazionesha na kuzitangaza biashara zetu. Tizama njia za kutangaza biashara bila gharama lakini kwa kutumia ubunifu na nidhamu.
1.Hakikisha unaweka furaha kwa wateja ulionao sasa.
Ni tabia ya wafanyabiashara wengi kuwachukulia poa wateja walionao na kuamini kuwa ili wafanikishe malengo yao wanahitaji wateja wapya, mteja mpya anapokuja kununua kwako moja ya jambo analofanya ni kuwasiliana na wateja wako wa sasa. Mitandao ya kijamii imekua vilimge vipya kwa sasa, kila siku watu wanajadili namna kampuni zinavyowahudumia na ubora wa huduma. Wafanye wateja wako ulionao wakuzungumzie vizuri wawe mabalozi wa biashara yako, utajikuta unatangaza biashara yako bila kulipia chochote.
Soma: Matangazo pekee sio msaada kama haujali wateja.2.Tumia mikusanyiko ya watu kueleza namna biashara yako inavyoweza kutatua matatizo yao.
Asilimia kubwa hatupendi kusomewa matangazo, lakini huwa tupo tayari kuacha shughuli zetu kumtafuta mtu anayeweza kutatua matatizo yetu. Unapopata sehemu ya kuzungumza kwepa kutumia lugha za kutangaza, badala yake tumia lugha za kuonesha unavyoweza kutatua tatizo la mtu. Elezea ulivyokutana na mteja wako wa kwanza au huyo uliyenaye sasa, alikua na tatizo la aina gani na ulimsaidiaje kulitatua tatizo lake. Kama utaweza kuwa msimuliaji mzuri utaweza kukwepa gharama nyingi za matangazo kwa kutumia nafasi unazopata kungumza.
3.Saidia vikundi na shughuli za kijamii.
Kuna msemo maarufu unaosema, tarajia kufanyiwa kile unachowafanyia wengine. Kila mmoja katika eneo lake vipo vikundi na shughuli mbali mbali za kijamii, tumia sehemu hizo kutoa msaada . Watu watashawishika na watakua mabalozi wako kwa kuelezea kile ulichowasaidia. Hudhuria kwenye mahafari ya shule mbali mbali ambazo unajua wazazi wao ni kundi la wateja unalotafuta, toa zawadi kwa wanafunzi au walimu. Zipo njia nyingi zaidi za kutoa misaada kwenye vikundi vya kijamii.
4.Shirikiana na wafanyabiashara wengine.
Watu wamekua wakitafsiri vibaya kuhusu ushindani, ushindani sio uadui. Shirikiana na wafanyabiashara wenzio katika mambo yanayohusu biashara zenu. Kuna nafasi kubwa ya kuitangaza biashara yako kama utashirikiana na wafanyabiashara wengine. Kuna umoja wa wafanyabiashara nenda kajiunge, biashara nyingine inahitaji msaada toka kwako saidia. Licha ya kupunguza uhasama pia utapata nafasi ya kujua namna biashara zingine zinvyoendeshwa.
5.Tengeneza bidhaa na huduma kulingana na mahitaji ya soko lako.
Huduma isiyokidhi haja ya mteja inatosha kabisa kuibomoa biashara yako, hakuna mtu anayependa kupoteza pesa au muda kwenye bidhaa asiyofurahia. Kuipa biashara yako uhakika wa kutangazwa bila gharama inakuhitaji uzalishe bidhaa zinazohitajika na kukidhi mahitaji ya soko lako. Ingawa sio bidhaa zote zinazo ongoza sokoni ni bora lakini bidhaa bora ni silaha ya kwanza kwako kuweza kutangazwa na wateja bila ya kutumia nguvu kubwa. Ili uweze kupata bidhaa bora inakuhitaji kushirikisha wateja kabla ya kutengeneza au kuzalisha huduma mpya.


