Mwanzo wa biashara kuna vitu vingi vya kukatisha tamaa ambavyo kama hauna ujasiri ni rahisi kuona hauna kipaji au bahati na biashara lakini sio kweli. Kuna tofauti ya kufanya biashara ukiwa na kazi nyingine inayokupa kipato, na kufanya biashara kisha ukategemea hapo hapo nauli, chakula na Panaldo ukiumwa. Sasa ipi ni njia sahihi ya kuendesha biashara katika mazingira ya namna hii?
Kwanza usifanye biashara kwa kivuli cha wewe ni Bosi, fanya biashara ukiwa kama kijakazi.
Hapa ni kuanzia kwenye maamuzi, kujituma na matumizi ya pesa, jione kama vile ni kijakazi na kuna bosi mwenye maamuzi zaidi kwenye hiyo biashara, najua bado unajiuliza kivipi. Ukifungua biashara jiweke kama kibarua, jiulize kama ni kibarua ningekua namlipa shilingi ngapi kila siku?
Chukulia mauzo ni mabaya, halafu kijakazi anakwambia anataka pesa yake mliyokubaliana je ungetumia njia gani ili akuelewe? Lazima ungemuomba, mdogo wangu leo biashara sio nzuri naomba nikupe nauli tu kisha tuangalie kesho itakavyokua. Wakati wote unapojiona unahitaji kufanya matumizi lakini biashara ni mbaya jiweke kwenye nafasi ya kijakazi hapa utakua na uwezo wa kuituliza akili yako na kupata huruma dhidi biashara yako.
Unapohitaji kula lakini haujafanya mauzo yoyote, angalia watu wanaokuzunguka na uwatumie kukidhi haja yako, sio kweli ukose rafiki hata mmoja wa kwenda kula kwake kwa usiku mmoja kisha utizame kesho itakuaje. Ingawa hili nalo linategemea mtaji wa watu, lakini maana iliyopo hapa ni kuwa biashara ni kama rafiki tu, rafiki hana jukumu la kukulisha kila siku, siku akishindwa mtafute rafiki mwingine.
Unahitaji pesa ya dawa na biashara haina mauzo ya kukupa faida, angalia watu ulionao pembeni na utafute msaada kwao, hata siku moja usiwe muoga kuomba msaada pale unapozidiwa, kiongozi mzuri ni yule aliye muwazi na kukubali kuwa anahitaji kusaidiwa. Zipo changamoto nyingi za kufanya biashara bila ya kuwa na kazi nyingine, lakini ukiweza kuimudu hali hio wewe ndio utakua mfanyabiashara wa kweli.
Hitimisho
Biashara yako ni kama rafiki wa kawaida, sio kila wakati utegemee yenyewe peke yake ndio ikupe msaada wa mambo yako. Fikiria marafiki wengine ulionao. Tatizo tukianzisha biashara ndio tunaona biashara inamajukumu yote ya kutulea na kutusaidia. Mwisho wa siku tunakula mtaji.
Biashara ni rafiki kama marafiki wengine, biashara sio Ajira, Mshahara wa Ajira ndio unautegemea kufanya kila kitu. Lakini biashara inakusaidia pale tu inapoweza kama vile rafiki, kuna muda anasema hana tafuta pengine na biashara ni hivyo hivyo.


