Biashara tano za kujifunza na kujaribu Mwaka 2020 ndani ya Jiji la Dar es salaam.

https://www.waziriconcept.com/2020/02/biashara-tano-za-kujifunza-na-kujaribu.html

Umewahi kumsikia mtu akisema anayo pesa lakini haoni biashara ya kufanya, kuchagua na kuamua biashara ni moja kati ya maamuzi magumu kwenye kuanza safari ya Ujasiriamali.

Kufanya swali hili kuwa jepesi kwako, hizi ni fursa tano unazoweza kuweka juhudi na pesa zako kwa mwaka 2020 ndani ya Dar es salaam, na popote palipo na mazingira rafiki.

1.Sekta ya vyakula vya asili vyenye kulinda afya (Vyakula tiba).
Kwa mujibu wa shirika la afya duniani (WHO) ongezeko la vifo vitokanavyo na magonjwa yasiyo ya kuambukiza limekua ni kubwa ambapo kwa Tanzania kati ya Asilimia 18 hadi 24 ya vifo vinatokana na magonjwa hayo, Saratani, Kisukari na Matatizo ya moyo. Tofauti na miaka 10 iliyopita, hivi sasa kumekua na kundi kubwa linalopigania kuboresha afya zao katika vituo mbali mbali vya mazoezi.

Watu wengi wanajaribu kubadilisha mitindo yao ya maisha ikiwa pamoja na ulaji wa vyakula vya asili na vyakula tiba. Migahawa inayotoa vyakula visivyokua na mafuta, nafaka zisizo kobolewa, mboga mboga na matunda ni fursa kubwa kwa atakayeweza kuangaza kama tunavyo angaza.

2.Huduma ya usambazaji wa mizigo na vifurushi ndani ya mji.
Dar es salaam ndio jiji kubwa zaidi Afrika Mashariki, Jiji la 7 kwa ukubwa Barani Afrika. Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012, Dar es salaam inawakazi zaidi ya Milioni 4. Licha ya uwepo wa mabasi yaendayo kasi lakini bado usafiri wa kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine imekua changamoto.

Inazaliwa fursa kwa wajasiriamali kuzisaidia taasisi na biashara zinazouza bidhaa mbali mbali na kusambaza vifurushi kwa niaba, zipo tayari baadhi ya kampuni zinazotoa huduma ya usambazaji wa vifurushi, lakini bado mahitaji ni makubwa.

Bado zinatakiwa kampuni za kuja kuamsha sekta hii ya usambazaji vifurushi kwa kutoa huduma ya haraka zaidi lakini pia itayokua nafuu ili kuwapa faida wafanyabiashara na wanunuzi wa bidhaa mbali mbali.

3.Duka na uwakala wa nishati ya Gesi.
Katika hili kila mmoja anakua shuhuda kwa namna ambavyo matumizi ya gesi yamekua hayakwepeki kwa sasa. Kwenye kipindi kifupi zimezaliwa kampuni nyingi za kuuza gesi hapa nchini, kampuni hizo mpya na kongwe zote zinahitaji mawakala ili kuwafikia wateja wao kwa urahisi zaidi. Duka la gesi ni fursa unayoweza kuanza nayo kwa mtaji mdogo hata wa mtungi mmoja.

Unachotakiwa ni kujua katika mazingira yako kampuni gani rahisi kuingia nayo makubaliano lakini hakikisha pia inawateja wa kutosha, kampuni inayofanya juhudi kujitangaza zaidi na sio zile zilizolala.
4.Kununua Mahindi na kuyageuza kuwa Unga na pumba.
Kwa bahati mbaya sana kumekua na tabia ya kuiga biashara bila ya kujiridhisha na maamuzi, watu wengi wamekua wakiamini kuwa biashara ya mchele inalipa zaidi kuliko unga kupelekea hata wengine kuingia kwenye hasara wasizotarajia.

Ugali unabaki kuwa chakula mama kwa watanzania, ugali unaliwa na familia ya kipato chohote kile. Lakini kubwa nalokwambia ni kuwa, hatari ya kuchagua mahindi bora ni ndogo kuliko hatari ya kuchagua mpunga au mchele bora. Kingine zaidi ni kuwa, ili upate faida kwenye biashara ya mchele unahitaji mtaji mkubwa wa kuanzia wakati kwenye biashara ya unga na mahindi ni tofauti kabisa.

Kuongezeka kwa wafugaji kunazidi kutoa fursa kwenye biashara ya mahindi na unga, wakati ukiziacha pumba za mpunga shamba, pumba za mahindi bado zinakua ni faida. Kama biashara zingine, kabla hujaanza tizama kwanza hali ya soko unalotaka kuhudumia na ufahamu utapata wapi mahindi kwa bei nzuri na usafiri mwepesi.

5.Uwakala na usambazaji wa maziwa Fresh.
Nilitaka hii iwe ni Fursa namba moja lakini imekua ya tano kwenye huu mpangilio. Kama nilivyosema hapo mwanzo, watu wanapambana kujenga na kuboresha afya zao. Maziwa ni kitu chenye fursa kubwa ndani ya Jiji la Dar es salaam kwakua bado maziwa fresh hayajaingiliwa kama ilivyo kwa maziwa mtindi ambayo viwanda vingi ndio wanayazalisha.

Kama utapata Jokofu na Vyombo vizuri vya kusafirishia. Chukua oda katika Appartment za Mjini na maeneo yanayofikika. Tafuta chanzo chako bora cha kupata maziwa mazuri na masafi, amini kwamba utakuja kushangaa kwanini ulichelewa kuanza. Pia unaweza kufungua MILK BAR, weka maziwa yenye ladha mbali mbali, weka sehemu za kukaa na vitafunwa.

Hitimisho,
Akili za kuambiwa changanya na zako, pitia fursa moja moja na utizame inayoendana na malengo yako.Unaweza kuanza mtaji ambao wewe unaona unaweza kuupata, kila fursa katika hizi unaweza kuanza kidogo na sio lazima upate mtaji mkubwa.