Kwenye maamuzi ya biashara nani anayetangulia kati ya mteja na mshindani wako.


Ukiweza kujibu maswali ya aina hii kwa ufasaha unajiweka katika kundi la biashara zilizofanikiwa. Huwezi kufanikiwa kwenye biashara kama hauna uwezo wa kujiuliza maswali ya msingi kuhusu biashara na kuyatafutia majibu sahihi.

Wengi tunaweza kuwa tunafahamu maana ya Mteja, lakini tusiwe tunaelewa maana ya Mshindani.


Mshindani ni nani?
Zipo tafsiri na maana nyingi kuhusu ushindani lakini maana rahisi zaidi, ni biashara au kampuni unayochangia nayo maslahi ya kibiashara. Mshindani anaweza kuwa yule mnayenunua rasilimali sehemu moja, mnauza bidhaa sehemu moja, mnazalisha bidhaa aina moja.

Huwezi kumjua mshindani wako bila ya kumjua kwanza mteja wako ni nani, hili ni kosa lingine ambalo biashara nyingi hulifanya. Watu wanapotaka kuanzisha biashara huenda moja kwa moja kujiuliza nani anafanya biashara kama yake, akisha mjua anaanza kumuiga au kushindana naye bila kujua aina ya wateja ambao mwenzie amelenga.

Sasa ipi ni njia sahihi?
Baada ya kupata wazo la biashara anza kwa kuchagua aina ya wateja ambao unahitaji kuhudumia, unachohitaji ni kufahamu uwezo wako kama unaendana na mahitaji na sifa za wateja husika.
Baada ya kumjua mteja ndio utaanza kumchunguza na kujua wapi ananunua bidhaa zake kwa sasa, hapo ndipo utajua biashara inayouza bidhaa kama yako kwa mteja wako. Huyo ndio mshindani wako.

Nafanyaje maamuzi ya biashara?
Maamuzi ya biashara yanaanza kwenye tabia za mteja, anaweza asikwambie upunguze bei lakini tabia yake ikawa inakulazimu kupunguza bei. Wakati mwingine vitendo vya mshindani vinaweza visikulazimishe kufanya maamuzi kwa sababu tabia za mteja ndio kitu muhimu katika soko. Biashara bora haitizami nini mshindani wake anafanya, hutizama nini mteja anahitaji kwa wakati husika.

Ingawa ni kweli unapaswa kuwatizama washindani wako ili kujua upo katika nafasi gani, lakini maamuzi yanatakiwa yatokane na tabia za wateja katika manunuzi na mrejesho wanaokupa. Mshindani wako anaweza kuwa sababu ya kuibadilisha tabia ya mteja wako, hivyo wakati wote inakubidi uwe makini na tabia za mteja.