Jambo lenye thamani zaidi kwa mteja.


Unapowaza kuhusu tabia za wateja, anza kufikiria tabia zako wewe mwenyewe unapofanya manunuzi sehemu zingine. Zipo tabia zinazobadilika kutokana na umri, kazi, mazingira, asili na kipato lakini lipo jambo ambalo wateja wa aina zote hulipa thamani zaidi.

Huduma bora na kusikilizwa kwa wakati.

Sote tujiulize ni nani ambaye yupo tayari kupewa huduma mbovu kwa sababu atapata punguzo la bei? Umepanga utumie nusu saa kula chakula cha mchana, lakini umefika kwenye mgahawa muhudumu yupo bize kwenye Instagram anamuangalia Diamond Platnumz. Je, utaendelea kusubiri kwa sababu bei yao ni rahisi au utatoka kwa hasira na kwenda kula sehemu nyingine ili uendelee na ratiba zako.

Hivi ndivyo ambavyo biashara nyingi zinapoteza sifa za kiushindani kwa kutojali wateja kwa sababu wanauza bei rahisi. Hata kama bidhaa au huduma unayotoa ni bora lakini kama kiwango cha kuwasikiliza wateja ni kibovu, fahamu kuwa hamna unalofanya zaidi ya kujifukia mwenyewe. Mtoto huitwa ameshindikana tabia inapofika hatua ya kusemwa vibaya hata na mama yake mzazi, unadhani mpita njia atakuamini vipi kama wateja wako wanasema vibaya kuhusu wewe kila kona?

Bidhaa bora, bei nafuu, viendelee kubaki kuwa kama vitu vya kupunguza ushindani sokoni, lakini kivutio cha kweli kwa wateja ni huduma bora na kuwasikiliza kwa wakati. Hakuna mtu ambaye yupo tayari kupoteza muda kwa sababu bidhaa yako nzuri au bei yako ni rahisi, uzuri na urahisi ni mambo yaliyojificha lakini huduma mbovu huwa haina pazia.