Malengo ukishindwa kuyatimiza yatabaki kuwa mzigo wa ahadi wenye kukupa mawazo na mfadhaiko. Ili kuongeza uzalishaji, wapo washauri wanaoshauri kuamka mapema kila siku kabla dunia haijaaamka, wengine wanashauri tule vizuri, madaktari nao wanatushauri kufanya mazoezi.
Wapo wanayofanya yote hayo lakini bado wanajikuta wamebeba mzigo wa mawazo kwakua bado mambo hayaendi kama walivyopanga. Haya ni mambo saba yatakayo badilisha utendaji wako wa kazi na kufanya uongeze uzalishaji.
1.Ongeza ufanisi.
Kumbuka ni muhimu kuweka orodha ya mambo ya kutimiza ndani ya kipindi husika huku ukionesha chenye umuhimu na haraka, na kile kinachoweza kusubiri. Kwa kufanya hivyo utaweza kuyapa muda wa kutosha mambo yenye umuhimu yanayo hitaji utatuzi wa haraka.
2.Jifunze kutumia watu wengine.
Kweli kuna hatari kubwa kuziacha baadhi ya shughuli mikononi kwa watu wengine. Kama kweli unahitaji kuongeza uzalishaji lazima uwe na watu unaoweza kuwaamini na kuwapa baadhi ya majukumu. Jambo hili lina hatari hivyo hakikisha unayemkabidhi unapata muda wa kumkagua.
3.Tumia nyezo na vifaa vilivyo bora katika kazi zako.
Kuna muda mwingi na pesa nyingi huwa tunazipoteza pale tunapojifanya tunapunguza gharama, unaweza kutunza na kuokoa muda mwingi kwa kupanda bajaji kuliko kupanda daladala, lakini unaamini bajaji kwako ni gharama. Kama unajua Printer za ofisini kwako zinafanya kazi taratibu huna budi kubadilisha Printer ili uweze kufanya kazi nyingi zaidi. Vitendea kazi vilivyo chini ya kiwango humnyima mtu uwezo wa kukamilisha kazi ndani ya wakati.
4.Weka mipango yenye uhalisia, inayoweza kupimika.
Tatizo lingine kubwa ni kutokua na mipango yenye uhalisia, unashindwa kujua kwamba unaenda vizuri au vibaya sababu mwanzoni hapakuwa na mipango yenye uhalisia. Ainisha matokeo yatakayo kuonesha unakwenda vizuri. Mfano, kila mwezi nipate wateja wapya 50, kabla ya mwezi kuisha utajua utendaji kazi wako unakwenda vizuri au vibaya, utachukua tahadhari mapema na utajua wapi hujapafanyia kazi ilivyopaswa kuwa.
5.Zuia mambo yanayoharibu muda au kukutoa mchezoni.
Kama unasema saa tatu zijazo nitakua nafanya kazi fulani basi weka kando vitu vitakavyo haribu muda wako. Mitandao ya kijamii inaweza kuwa kikwazo kikubwa cha kutimiza malengo yako, haina maana usitumie simu lakini iweke mbali unapokua katika kazi husika.
6.Jipongeze baada ya kutimiza malengo yako japo kwa uchache.
Wakati unatafuta maisha usisahau kuishi, jipongeze pale unapofanikisha malengo yako. Tafuta mgahawa unaopenda, nenda kale chakula unachokipenda huku ukiiambia nafsi yako kuwa unajipongeza kwa mazuri uliyotimiza, kama kuna Movie nzuri unaipenda nenda kaiangalie huku ukiieleza nafsi yako kuwa unajipongeza.
7.Boresha mazingira unayofanyia kazi zako.
Kufanya kazi kwa ufanisi kunahitaji mazingira yaliyo rafiki kwa kile unachokifanya, kama kelele ni tatizo kaa nazo mbali, joto linalofaa kwenye sehemu ya kazi ni nyuzi joto 20-21 C. Joto lililozidi huleta usumbufu na karaha ni vema kufanyia kazi zako mazingira rafiki ili kuepuka upotevu wa muda.
Hitimisho;
Inawezekana moja kati ya haya ndio changamoto kwako, usidharau jitathimini upya na ufanye mabadiliko. Kutotimiza malengo sio ishara ya uvivu, kuna mazingira huwa yanakulazimisha kutomaliza kazi kwa wakati. Kama ni vitu unavyoweza kuboresha usiache kufanya hivyo, malengo yasiyo timia hubakia kuwa madeni kwenye akili zetu yenye kutuachia mawazo.