Tunachotakiwa kuwaza ni namna gani biashara zetu zitaonekana na kuaminika, kadiri unavyozidi kuonekana ndivyo watu watazidi kukuamini na kutambua uwepo wako. Ili uweze kupata wateja lazima kwanza utengeneze nafasi ya wao kukuamini, ni ngumu mtu kuamini kitu asichokiona wala kutambua kama kipo. Bahati mbaya wafanyabiashara wanasahau kujiuliza swali la msingi kabisa mwanzoni wakati wanaanza, Nitaenda kuonekana kwa kutumia njia gani?
Zipo njia tofauti za kuonekana lakini zinaingia kwenye makundi mawili, Njia za asilia na Njia za kidigitali. Hapa utachagua kulingana na aina ya biashara unayofanya, rasilimali ulizonazo na wateja unaotaka wakufahamu. Huwa nasikitika sana kuona wafanyabiashara wanalazimisha kufanya promosheni kwenye majukwaa ambayo hata wateja wao hawapatikani huko. Kabla hujachugua njia ya kutumia kuonesha biashara yako anza kujua kwanza watu gani unataka kuzungumza nao.
Njia asilia za kuonesha biashara yako na kupata nafasi ya kuaminika.
1.Sajili biashara yako na ipate uhalali sokoni.
Kumbuka unataka uonekane na watu wakuamini ili uweze kuwauzia, sasa itakuaje kama unachokiuza hakina vibali na wala hakitambuliki na mamlaka zinazosimamia bidhaa na huduma za aina hiyo? Utakua mwanzo wa kujificha na kutopata nafasi za kuonekana. Kusajili biashara linatakiwa kuwa wazo lako la kwanza kabla hujafikiria kodi ya ofisi na mengineyo. Bidhaa iliyosjiliwa inayo nafasi kubwa ya kupata mawakala kuliko isiyo sajiliwa.
2.Weka ufadhili kwenye matukio yanayofanyika kwenye Jamii uliyonayo.
Hapa utapata nafasi ya kuonesha biashara yako kwa gharama nafuu isiyo umiza, utapata nafasi ya kuonesha biashara yako bila ya kutumia kiwango kikubwa cha pesa. Utajumuika na jamii yako na wao watakufahamu na watapendezwa kuona unashirikiana nao katika mambo yao. Ili ufanikiwe hakikisha unaweka udhamini kwenye matukio yanayoleta watu unaowataka. Sio tangazo la bia unapeleka kwenye tamasha la watoto.
3.Tumia mawakala kusambaza bidhaa unayo uza au huduma.
Kama unauza bidhaa hakikisha inapata vibali vyote na kuipa uhalali sokoni, angalia maduka yanayosambaza bidhaa kama yako kisha nenda kawape punguzo la bei ili nao wauze bei ya juu zaidi. Hapa unao uwezo wa kuongeza nafasi ya kuonekana kwa kadiri utakavyo wewe mwenyewe. Kama utahitaji upate watu 1000 kwa mwezi unaweza kutafuta maduka 10 kisha kila duka likakupa watu 100.
4.Vipeperushi na Mabango kwenye mikusanyiko mikubwa.
Tumia vipeperushi kusambaza sehemu zenye mikusanyiko na kuwapa watu wanao kuzunguka. Hapa napo ujumbe ni jambo muhimu la kuzingatia weka ujumbe unao eleweka na picha za kuvutia. Kama bajeti yako inaweza kuweka mabango, yenyewe pia ni njia bora.
5.Tumia marafiki, jamaa na watu wanao kuzunguka.
Tengeneza nguo zinazobeba ujumbe wa biashara yako, Calendar, Vikombe, Vipeperushi na uwasambazie watu wako wa karibu ambao unajua wanamtandao mzuri wa watu.
Njia za kidigitali za kuonesha biashara yako na kupata nafasi ya kuaminika.
Mapinduzi ya mtandao yamekuja na mambo mengi ambayo mfanyabiashara ni ngumu sana kuyakwepa kwa sababu watumiaji ndio wanashinda humo. Ujio wa Google, Twitter, Facebook, Whatsapp, Telegram, Youtube, Tiktok, Pinterest, Linkedin na mengine mengi yamefanya sasa biashara zibadilishe mitazamo na kujifunza namna ya kuziweka biashara zao kwenye ulimwengu wa digitali. Biashara inaweza kuongeza nafasi yake ya kuonekana kwa kufanya mambo yafuatayo.
1.Weka biashara yako kwenye Ramani za google.
Kupitia Google My Business utaonesha mtaa ambao biashara yako ipo, Mawasiliano yako, saa za kazi, huduma unazotoa, picha na muonekano wa biashara, bei za bidhaa na huduma za ziada. Tafuta mtu anayeweza kukuwekea biashara yako katika ramani za google au unaweza kutueleza hata sisi tutakusaidia kufanya hilo. Google My Business itawezesha biashara yako kuonekana pale watu wanapotafuta huduma kama yako mtandaoni na kuoneshwa biashara yako.
2.Fungua Ukurasa kwenye mtandao unaotumika na watu wako.
Facebook inaweza kuwa bora kwangu lakini isiwe bora kwako, Twitter inaweza kuwa bora kwako lakini inaweza isiwe bora kwa mtu mwingine. Jambo la kuzingatia unapofungua ukurasa wa biashara ni aina ya watu unaotaka kuwafikia wapo katika mtandao upi, lakini kwa sababu tunahitaji kuonekana zaidi ni vema kuchagua sehemu siyo chini ya tatu kisha ukawa unatizama wapi panatoa matokeo mazuri ndipo unapoongeza nguvu huko.
3.Tengeneza Website iliyo bora na uitangaze.
Hakikisha Website unayotengeneza inawakilisha vema biashara yenu kwa maana inakua na taarifa zote muhimu na inarekebishwa kila wakati mnapofanya mabadiliko kwenye huduma na bidhaa zenu. Ukiweka namba ya simu kwenye website hakikisha ndio hiyo hiyo namba ya biashara.
4.Tumia watu wenye ushawishi kwenye mitandao ya kijamii.
Kumpa mtu ujmbe wako bure akuwekee kwenye ukurasa wake hilo haliwezekani, lakini ukiweka malipo na yeye anavyoweza kufaidika hilo ni zoezi jepesi. Njia hii imekua ni maarufu sana kipindi hiki na badala ya kutumia watu wenye gharama kubwa, unaweza kuwachagua watu wa kati ambao wanao watu watakaoweza kukupa matokeo chanya.
Hitimisho,
Biashara ni kujifunza na kuwa mbunifu kila siku inayoitwa leo, zipo njia nyingi lakini hizi ni njia bora za kuanza nazo. Ni njia ambazo hazitaki uwe na mtu wa masoko kwenye biashara yako, ni wewe mwenyewe unaweza kufanya vyote hivi. Hilo ndio lengo la Waziri Concept, kutatua matatizo makubwa bila maumivu.