Sokoni siyo sehemu ya kupiga Ramli, ingiza biashara sokoni ukiwa unajua nini unafanya.


Kuingiza biashara sokoni bila kuwa na taarifa muhimu ni kujiweka kwenye mazingira ya hasara mapema kabisa. Tukianza kujadili kiasi cha pesa kinachotumika na kampuni zilizoendelea katika kufanya tafiti na majaribio tunaweza tusielewane, kwa sababu utajiuliza wanawezaje kutumia kiasi kikubwa cha pesa namna hiyo na zinarudi vipi kwao.

Mafanikio ya biashara yanategemea kwa kiasi kikubwa taarifa sahihi. Zifuatazo ni taarifa ambazo kila biashara inatakiwa kuzijua kabla ya kuingiza biashara sokoni.

Aina gani ya tatizo biashara yako inaenda kutatua
Watu wanatumia pesa kutatua matatizo yao ambayo ndio hayo tunayaita mahitaji, kabla hujaingiza biashara sokoni ni lazima uweze kufahamu aina ya tatizo ambalo utaenda kutatua na kama tatizo hilo litawalazimisha watu kutumia pesa zao kwako. Biashara ili iweze kukua inahitaji mapato ya kuwezesha kuendesha shughuli zake, mapato hayo ni pesa.

Kikundi gani cha watu unachoenda kuuza kwao
Kila biashara iliyoendelea kuna kundi la watu ambao imelenga kuwafikia kisha wengine wanakua ni ziada. Kufahamu watu utakao wauzia itakuondolea usumbufu wa kutaka kumuuzia kila mtu. Itakua ni rahisi kuandaa bidhaa, kuandaa matangazo pia hata eneo la kuweka au kuongeza ofisi baada ya kujua watu gani ambao unawahitaji kulingana na tatizo unalotaka kulitatua na kutizama uwezo wako.

Mahitaji ya kisheria kwenye biashara yako
Popote duniani kuna misingi ya sheria inayotoa ruhusa na vibali vya biashara, usifanye maamuzi kwa kutumia maneno ya kuambiwa peke yake, kama unataka biashara ikue basi fuatilia mahitaji ya kisheria kwenye biashara unayotaka kuanzisha. Kufanya hivyo itakupa mwanya wa kupata taarifa kuhusu biashara zingine zinazofanana na biashara yako, pia inakupa uhakika wa kudumu kwenye soko bila hofu kuhusu kesho yako.

Wajue vizuri washindani wako na uelewe biashara zao
Mara nyingi biashara ambazo tunaziweka sokoni huwa tayari ziliwahi kufanyika hapo nyuma au zinafanyika sasa, yakupasa uzijue angalau biashara tatu zinazofanana na wazo lako kisha ufanye tathimini ya vile wanavyo endesha biashara zao hapo ulipo wewe. Kwa kufanya hayo utajua kitu cha kuongeza na kupunguza ili uweze kuwa tofauti na wao.

Fahamu vyanzo vya mapato vitakavyo kusogeza muda unaosubiri faida
Kosa linalofanyika ni kufikiria kwamba faida inapatikana mwezi wa kwanza baada ya kuweka biashara sokoni. Hili ni kosa ambalo biashara nyingi hulifanya, unapoingiza biashara sokoni inahitaji muda usiopungua mwaka mmoja ndipo uweze kuhesabu faida ya moja kwa moja. Mwanzoni kabisa inakubidi ujue vyanzo vyako vya mapato vitakavyo kuwezesha kuendesha mahitaji ya kila siku ya biashara.

Hitimisho
Ingawa inafahamika kuwa biashara ni shughuli yenye maamuzi magumu na yenye hatari, lakini hatari yenyewe inatakiwa kupigiwa hesabu. Hakikisha unapata taarifa za uhakika kabla ya kuingiza biashara sokoni, usifanye maamuzi kwa habari za kusikia peke yake bila kufatilia.