Haijalishi biashara yako kubwa kiasi gani, uaminifu sio jambo linalokuja kwa usiku mmoja, ili wateja waweze kukuamini inahitaji utumie akili na nguvu za ziada. Uaminifu haupatikani bure bure kwa kufungua tu duka kisha kujaza vitu dukani, usitegemee wateja watakuelewa kwakua eti unaweka matangazo Instagram na Facebook.
Kwanini watu wameiamini Halotel haraka kuliko Zantel? Zitaelezwa sababu nyingi, lakini kama wewe mwenyewe hujamchagua mtu wa kukuamini basi hakuna atakayekuamini.
Unahitaji watu wa aina gani wanunue biashara yako, Ili watu wakuamini lazima wewe mwenyewe uchague njia ya kupita. Tigo walikua wanaitwa mtandao wa wanafunzi miaka ya 2006/2007, Vodacom walifahamika mtando wa wafanyabiashara, Halotel Mtandao wa vijijini, biashara yako inawahusu watu gani?
Kama wateja wako ni Wanafunzi hakikisha unakuwa nao karibu muda wote na unajitokeza kwenye shughuli zao za kila siku. Haitoshi kwa kusema peke yake kuwa wateja wako ni kundi fulani eti kwa sababu unaweka bidhaa au huduma za aina yao. Kama unalenga kuhudumia kundi fulani hakikisha unaonekana na kundi hilo hadi litambue kuwa wewe ndio mtu wao wa kukufuata. Hapo ndipo unaweza kutengeneza uaminifu kwa wateja ulio walenga.
Lakini hayo yote yatawezekana endapo utaweka mpango kazi na sio kwenda kichwa kichwa (Strategy). Kwenye mpango kazi utaonesha kundi gani unalifukuzia, mahitaji yao, uwezo wako, bajeti na mbinu utakazotumia, washindani wenzio, lengo unalotaka kutimiza na muda utakaotumia kukamilisha malengo.
Hitimisho;
Usitegemee kuingia kwenye biashara ndani ya mwezi mmoja tayari watu wakufahamu na wakuamini, hakuna biashara ya hivyo dunia nzima. Watu kukuamini inahitaji uvumilivu huku ukiboresha huduma zako mara kwa mara. Endelea Kupambana.


