Zijue njia bora za kutangaza biashara bila ya maumivu unapokua na mtaji mdogo.


Mfanyabiashara huwa anabaki njia panda pale ambapo anahitaji kufanya maamuzi lakini mtaji wake haumpi fursa. Binafsi nakutana na vilio vingi vya aina hii, unamshauri mfanyabiashara kuchukua hatua fulani ili aweze kuisogeza mbele biashara yake lakini unakuta changamoto ni mtaji alionao.
Lakini kwenye changamoto lazima kunakua na njia mbadala za kuweza kuitatua changamoto husika,  kwakua mtaji wako ni mdogo haina maana ndio huwezi kufanya maamuzi.

Hizi ni njia bora za kutangaza biashara bila ya maumivu unapokua na mtaji mdogo.

Tumia marafiki, ndugu na jamaa wa karibu ulionao,
Wakati mwingine huwa tunawaza kuhusu watu wa nje ikiwa tunao watu wa ndani ambao wanaweza kutimiza kile tunachohitaji, unaweza kuifikisha biashara yako mbali kwa kutumia marafiki na jamaa zako ambao mmekua na mahusuiano mazuri na wale ambao ulishawahi kuwasaidia. Kitu kikubwa kinacholipa kwenye huu ulimwengu ni kuwa mtu mwema kwa kadiri utakavyoweza, unaposaidia watu ndivyo unavyoongeza nafasi ya wewe kusaidiwa vile vile.

Vipeperushi, Business card sio vitu vya kuacha kuwa navyo,
Kwa aliye na mtaji mdogo au biashara changa kufanya Marketing ya kidigitali kumiliki Website na kutangaza mtandaoni inaweza kuwa ni changamoto kwake lakini njia hizi asilia ni rahisi sana. Kama utakua na vipeperushi maana yake utaweza kuwapa watu wako wa karibu niliotaja hapo mwanzo wakasaidia kukutangaza kufanya ujumbe wako ufike mbali zaidi.

Hudhuria Maonesho yote ya biashara yaliyo karibu na wewe,
Unaweza kukosa banda la maonesho kwenye viwanja vya Saba Saba au Nane Nane lakini unaweza kwenda na timu yako ikiwa imevaa sare ya biashara mkawa mnatawanya vipeperushi na kutumia mdomo kuzungumza na watu kuhusu biashara yenu na kuwaeleza vipi mnapatikana. Fanya hivyo hivyo kwenye shughuli zingine za kijamii unazopata mialiko au kuhudhuria.

Toa ushauri na ufundishe watu kuhusu kile unacho kiuza,
Kama nitajifunza kwako namna ya kupangilia mavazi unadhani itakua rahisi niende kununua nguo sehemu nyingine? Kama wewe ndiye utakua wa kwanza kunifundisha namna ya kutunza mboga zangu unadhani nitaenda wapi nakitaka kununua mboga? lazima nitakufata wewe kwasababu ndiye mtu ninaye kuamini. Haijalishi biashara gani unafanya, weka utaratibu wa kufundisha na kuelekeza watu namna ya kutatua matatizo yao.

Tengeneza bidhaa bora inayokidhi mahitaji ukisindikiza na huduma nzuri.
Kuna bidhaa zimekua maarufu sio kwa ajili ya matangazo mengi barabarani na redioni, zimekua maarufu kwa sababu zinakidhi mahitaji ya watumiaji na tumekua tukielekezana wenyewe ukitaka kiatu kikali nenda duka fulani. Biashara zingine zimekua maarufu kwa huduma zao nzuri zinapelekea watu wanaelekezana wenyewe, ukitaka kuhudumiwa haraka nenda saluni fulani.

Hitimisho,
Pesa sio kitu pekee kinachoweza kukusaidia kuitangaza biashara yako na kuisogeza mbele, zipo njia mbadala ambazo ukiziwekea juhudi na ubunifu ni rahisi kupata matokeo kuliko yule ambaye kalipia tangazo mtandaoni na halimpi wateja kwakua limekosa mvuto. Mfanyabiashara wa kweli pesa kwake sio tatizo, Mfanyabiashara wa kweli hutumia kichwa chake kuwaza na kutatua changamoto.