Zijue sababu tano zinazo zuia wateja kununua kwenye biashara yako na mambo gani ufanye ili ujinasue

Iwapo unafanya juhudi kubwa kutangaza biashara yako na kufanya harakati nyingi za kimasoko lakini haufikii wateja na kupata mauzo kama inavyopaswa kuwa, muhimu kufanya tathimini ujue kwanini na ufanye maboresho. Wanunuaji wote wanayo mahitaji na hatua ambazo hupitia kabla ya kufanya manunuzi. Kama matangazo yako na mbinu za kimasoko hazifiki vigezo vyao, moja kwa moja hiyo tayari ni sababu kwanini biashara yako haipati wateja kama unavyotaka.

Ukiweka kando swala la bei, wateja huvutiwa na faida iliyopo kwenye bidhaa wanayo nunua pamoja na uwezo wake wa kutatua mahitaji yao, ili mbinu zako za masoko ziwe zenye faida, wateja wanatakiwa kushawishika kwamba biashara yako inagusa mahitaji yao na yenye thamani kwao. Mfano unauza mgahawa, kwenye matangazo yako mteja anatakiwa ashawishike kuwa akija kwako tumbo lake litakua sehemu salama.

Kumshawishi mteja kuwa bidhaa yako inafaida ni rahisi kwa maneno kuliko vitendo. Fanya tathimini kwa kiasi gani utafanya mbinu za kimasoko kumbadilisha mnunuaji kuwa mteja kwako. Zipo sehemu tano unazoweza kuzifanyia mabadiliko na kuziongezea nguvu.

Biashara yako haitambuliki kwao

Mnunuaji yoyote yule hawezi kulipia bidhaa ambayo hana ufahamu nayo. Kama unatangaza biashara yako, lakini wanunuaji bado hawajitokezi kwako, sasa huo ni wakati wa kufanya tathimini ujue wapi kwenye tatizo. Anza kwa kujiuliza,  matangazo yako yanagusa watu sahihi?  Ujumbe wako unawapata watu ambao wako tayari kununua hiyo bidhaa yako? Muhimu kukumbuka kwamba dawa sio kufanya matangazo zaidi, kwa sababu tatizo litabaki kuwa ni wapi unayapeleka hayo matangazo, njia zipi unazotumia kutangaza hiyo biashara.

Anza kupitia watu wako ulio walenga na ufanye tafiti, mbinu zipi za kimasoko zitawafikia kwa usahihi na watakua tayari kununua kupitia njia hizo utakazo zitumia.

Watu hawakuelewi kwanini upo sokoni

Wanunuzi hawanunui bidhaa kwa kuangalia bei peke yake. Ndiyo wanafuata sana bei, lakini wananunua kwa kuangalia faida zipatikanazo kwenye bidhaa wanayo kwenda kununua. Ukiwauliza wateja wako faida tatu za bidhaa yako wataweza kukupa majibu sawa ? Kama ulikua hujui, hilo ni muhimu sana. Mbinu zako na kimasoko na matangazo zinatakiwa kulenga faida zinazopatikana kwenye bidhaa na biashara yako na sio bei peke yake.

Tengeneza orodha ya faida tatu zilizopo kwenye biashara yako na uzitumie kwenye kila tangazo na kila mbinu ya kimasoko.

Thamani yako haitambuliki

Neno thamani maana yake tathimini anayofanya mteja kwa kutizama mazuri ya biashara yako na uwezo wa kutatua mahitaji pamoja na matarajio yake kwa kulinganisha na biashara zingine zilizopo sokoni. Thamani yako itakua kubwa kwa kutegemea kiasi gani biashara yako inatatua zaidi mahitaji yake ukilinganisha na biashara zingine. Unaweza kutumia faida zilizopo kwenye biashara yako kutengeneza na kuonesha thamani ya biashara yako. Hiyo thamani ndio itakayo kuwezesha kuuza zaidi biashara yako.

Kama mteja haioni thamani ya biashara yako, tambua kuwa biashara yako ataiweka kando na kuzifuata zile zilizo na thamani kwake. Ili kuonesha thamani ya biashara yako kwenye matangazo, onesha watu wanavyotumia bidhaa yako na wanavyoielezea.

Hauna ulazima wowote ule kwa mteja

Wanunuzi wanajua kwamba biashara yako inakidhi haja zao?  Je inafanya maisha yao kuwa mepesi zaidi, inaokoa muda wao, inafanya wajisikie vizuri ? Biashara yako inakidhi haja gani? Usikae kimya waeleze wanunuzi wako. Usiwafanye wahisi au waje na majibu wao wenyewe. Waambie na uwasaidie kuwaelimisha kwanini wanatakiwa kutumia bidhaa yako.

Kama ambavyo tumesema mbinu za kimasoko zinatakiwa zieleze thamani ya biashara yako, hivyo hivyo unatakiwa uwaoneshe madhara ya kutotumia bidhaa yako ni makubwa kiasi gani.

Biashara yako inapatikana kwa shida sana

Wanunuzi hawawezi kunua bidhaa ambayo haipatikani kwao. Kama wanasikia kuhusu biashara yako lakini haipatikani kwa urahisi, sahau kuhusu kuuza.  Wanunuzi wanataka kuifikia na kuinunua bidhaa au biashara yako kwa urahisi. Utafanyaje ili iwe rahisi wao kuweza kuipata biashara yako?Kuiweka  maeneo tofauti tofauti? Kuwa na wasambazaji kila kona ya Mji? Kutangaza na kuuza kupitia mtandao? Fanya tathimini kwenye upatikanaji wa baishara yako na uangalie kama kunahitaji mabadiliko yoyote.

Tizama aina ya biashara yako na watu unaotaka kuwauzia. Kuna biashara zinafanya vizuri sana mtandaoni, lakini zingine zinahitaji mteja afike dukani aione ndio aweze kununua.

Hitimisho
Muhimu kwa mfanyabiashara kujua kuwa, ili uweze kufikia wateja kwa kiasi unacho kitarajia lazima kwanza ufahamu mteja gani unaye muhitaji. Sio kila mtu sokoni utaweza kumuuzia ila kila uliyelenga unaweza kumuuzia.